KUKOSA hamu ya tendo la ndoa kwa mwanamke kunaweza kutafsiriwa kwa aina tatu, ambazo ni kutopata hamasa ya kufanya tendo la ndoa hata b...
KUKOSA hamu ya tendo la ndoa kwa mwanamke kunaweza kutafsiriwa kwa aina
tatu, ambazo ni kutopata hamasa ya kufanya tendo la ndoa hata baada ya
kuchochewa; kuepuka kufanya tendo la ndoa ukiwa kwenye mahusiano bila
sababu ya msingi; kushiriki tendo la ndoa bila kufurahia na bila kufi
kia kilele.
Tatizo hili linaweza kuleta kutokuelewana baina ya wenza na ni chanzo
kimojawapo cha mafarakano kwenye mahusiano. Kama ilivyo kwenye ukosefu
wa nguvu za kiume, kukosa hamu ya kufanya tendo la ndoa kwa wanawake
kunasababishwa na matatizo ya kiafya au ya kisaikolojia.
Kunaweza kutokea baadhi ya nyakati kwa muda mfupi; lakini endapo tatizo
hilo linakuwa endelevu kiasi cha kusababisha matatizo kwenye uhusiano ni
vizuri kutafuta ushauri wa kitaalamu.
Mara nyingi kukosa hamu ya tendo la ndoa kwa wanawake kunaletwa na adha
au maudhi fulani ambayo yametokea na hayajazungumziwa baina ya wenza au
kutafutiwa ufumbuzi.
Hivyo, ushauri wa kwanza ni kuwa na mawasiliano ya wazi ili kurekebisha yale yanayowezekana.
Tendo la ndoa kwa mwanamke linahusisha vitu vingi lakini hasa ni
matayarisho ya kutosha yanayoleta hisia na vitendo vinavyoonesha
kupendwa, kuthaminiwa na hali ya kuwa salama.
Hamu ya tendo la ndoa haiji tu mara moja pale ambapo mwenza mmoja
amejisikia, bali mazingira lazima yawe sahihi na mazuri ili wote
kufurahia.
Sababu za kisaikolojia zinazoleta kukosa hamu ya kufanya tendo la ndoa
kwa mwanamke ni kama vile historia ya kufanyiwa vitendo viovu kama
kubakwa, kutokuwa karibu na mwenza kifikra, mawasiliano hafifu na
migogoro ya mara kwa mara kwenye uhusiano.
Sambamba na sababu hizo ni mazingira yasiyo rafiki kwa mfano uwepo wa
watoto au mkwe chumba cha karibu, pamoja na mwenza aliyelewa.
Zipo pia sababu za kiafya ambazo ni pamoja na maumivu wakati wa kufanya
tendo la ndoa, upungufu wa nguvu za kiume kwa mwenza, baadhi ya dawa,
pombe na mabadiliko ya homoni hasa pale mtu anapokaribia kukoma hedhi.
Hatua ya kwanza ya kuchukua endapo una tatizo la kukosa hamu ya kufanya
tendo la ndoa ni kutafuta ushauri wa kitaalamu ili kubaini endapo tatizo
lako ni la kiafya au la kisaikolojia. Mtaalamu wa afya atatoa ushauri
kulingana na tatizo atalogundua.
Asilimia kubwa ya matatizo ya kukosa hamu ya kufanya tendo la ndoa kwa
mwanamke yanaletwa na sababu za mahusiano, hivyo basi hatua ya muhimu
katika kukabiliana na tatizo hili ni kujadiliana na kufikia muafaka wa
mambo yanayowatatiza kama vile kukosa muda wa kukaa pamoja, mahusiano ya
kimapenzi na mtu mwingine ambayo yanaweza kuwa mapya au ya zamani na
malumbano ya mara kwa mara.
Ni muhimu kufahamu pia kuwa baadhi ya mambo nje ya mahusiano yanaweza
kuleta madhara kama vile matatizo ya kifedha au matatizo kazini.
Yote haya yanasababisha kukosa hamu ya kufanya tendo la ndoa na hivyo ni
muhimu sana kutafuta wataalamu wa ushauri ili kuweza kuzungumzia mambo
haya na kupata mbinu za jinsi ya kukabiliana nayo.
Kwa wale wenye shida za homoni zinazosababisha kukosa hamu ya tendo la
ndoa, mtaalamu wa afya atashauri njia bora ya tiba ikiwa ni pamoja na
kukupatia dawa za kurekebisha hali hiyo.
COMMENTS