Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU mkoa wa Katavi inamshikilia Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Kaulolo Taraf...
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa TAKUKURU mkoa wa Katavi inamshikilia Afisa Mtendaji wa
Kijiji cha Kaulolo Tarafa ya Inyonga Wilaya ya Mlele Mkoani
Katavi Kevin Elick Malenge kwa tuhuma za kumkamata akipokea
rushwa ya shilingi 150,000 kutoka kwa mkazi mmoja wa kijiji hicho
ili aweze kumruhusu kuishi na kufanya kazi ndani ya hifadhi ya
msitu.
Kaimu Kamanda wa TAKUKURU wa Mkoa
wa Katavi Cristopher Nakua alisema mtuhumiwa huyo
alikamatwa jana majira ya saa nne asubuhi katika eneo la
kijiji cha Kaulolo.
Alisema Mthumiwa Kevin alikamatwa
kufuatia TAKUKURU kupatiwa taarifa kutoka kwa msiri wao kuwa
afisa mtendaji huyo ameomba kiasi cha Tshs 200,000 kwa msiri
huyo ili aweze kumwingiza ndani ya hifadhi ya msitu ulipo
kwenye kijiji hicho ili aweze kuishi huko na kufanya shughuli
za kilimo .
Nakua alieleza kuwa baada ya
TAKUKURU kupata taarifa hizo ilianza kufanya uchunguzi na
kubaini kuwa afisa mtendaji huyo amekuwa akijihusisha na vitendo vya
kuomba na kupokea rushwa kwa watu mbalimbali kwa kupokea kiasi
cha kati ya Tshs 150,000 na Tshs 200,000 kwa lengo la kuwaingiza
watu kuishi ndani ya hifadhi ya msitu kinyume na sheria.
Baada ya TAKUKURU kubaini mpango huo
wa Afisa mtendaji wa Kijiji kuomba apatiwe rushwa ya shilingi
200,000 ndipo jana walipofanikiwa kumkamata mtuhumiwa akiwa
katika eneo la tukio akipokea rushwa ya Tshs 150,000.
Alisema baada ya mtuhumiwa
kukamatwa akipokea fedha alichukuliwa na maafisa wa TAKUKURU
kwa ajili ya mahojiano zaidi.
Kaimu Kamanda Nakua alisema
mtuhumiwa alikiri kupokea rushwa hiyo na uchunguzi umekamilika sasa
anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa ili kujibu
tuhuma zinazomkabii.
Katika hatua nyingine Kaimu Kamanda
Nakua ametoa wito kwa jamii kutojihusisha na vitendo vya kuomba na
kupokea au kutoa rushwa na haitasita kuwachukulia hatua wale wote
watakaojihusisha na vitendo vya rushwa hasa viongozi waliopewa thamana
na serikali kulinda rasilimali za Taifa na hifadhi zetu, kwa kufuata
kanuni taratibu na sheria za nchini.
COMMENTS