Aliyekuwa Kaimu Kamishna wa Madini, Ally Bondo Samaje amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka mawili ya mat...
Aliyekuwa Kaimu Kamishna wa Madini, Ally
Bondo Samaje amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu
mashtaka mawili ya matumizi mabaya ya madaraka.
Samaje amefikishwa katika mahakamani hiyo jijini Dar es Salaam leo Februari 9, 2018.
Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambna
na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu,
Victoria Nongwa kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo, April 9, 2013 na
Juni 21, 2013 Makao makuu ya Wizara ya Nishati na Madini.
Amesema akiwa Kaimu Kamishna wa Madini,
alitumia madaraka yake vibaya kwa kushindwa kuishauri Bodi ya Madini
katika utoaji wa leseni ya madini ya Graphite na Marble kwa Kampuni ya
Tanzaniteone Mining Limited na State Mining Corporation.
Katika shtaka la pili, April 16, 2013
makao Makuu ya Wizara ya Nishati iliyopo wilaya ya Ilala, akiwa Kaimu
Kamishna wa Madini na Katibu wa Bodi ya Ushauri wa Madini kutoka
wizarani, alitumia vibaya madaraka yake kwa kutoa maelekezo kwa msaidizi
wake John Nayopa kuandaa leseni za madini ya Graphite and Marble, bila
kufuata sheria ya madini.
Mshtakiwa yupo nje kwa dhamana baada ya
kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili na mmojawapo
kusaini bondi ya Sh 50milioni.
Pia mshtakiwa hatakiwi kusafiri nje ya nchi bila kibali cha Mahakama.
Na Hadija Jumanne, Mwananchi
COMMENTS