Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Stephen Magoiga (kushoto) akiwa na wataalamu Afisa Mipango, Mang’era Mang’era na...
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu,
Stephen Magoiga (kushoto) akiwa na wataalamu Afisa Mipango, Mang’era
Mang’era na Afisa Elimu Msingi Wilaya, Sostenes Mbwilo wakipata maelezo
kutoka kwa Afisa Elimu Ufundi, Moshi Balele kuhusu hatua za ujenzi wa
chumba cha darasa shule ya msingi Migunga unajengwa pia kupitia nguvu za
wananchi.
Mradi wa vyoo vya wanafunzi katika shule ya msingi
ukikaguliwa na maafisa elimu kutoka Halmashauri ukiwa katika hatua za
umaliziaji mbali ya kutumika kwa fedha za Serikali pia mradi huo
umechangiwa na nguvu kazi ya wananchi.
Sehemu ya vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Migunga
ikiendelea kujegwa katika shule ya msingi Migunga ikiwa ni muendelezo wa
mradi wa kuboresha huduma za sekta ya elimu.
Serikali ya Tanzania imeweka mkazo kuboresha mazingira ya
elimu kwa wanafunzi katika kujifunza ambayo ndiyo chachu ya mabadiliko
na kufanya sekta hiyo nyeti ipige hatua.
Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na ongezeko
la uandikishaji, kuleta usawa wa kijinsia kwenye shule za msingi na
sekondari nchini.Kumekuwa na changamoto mbalimbali
zinazoikabili sekta ya elimu na hivyo kufanya hamasa katika utendaji wa
walimu ishuke na vivyo hivyo kwa wanafunzi.
Ili kukabiliana na changamoto hizo, Serikali kupitia Ofisi ya
Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Wizara ya
Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa pamoja ikishirikiana na Mpango wa
Kuinua Ubora wa Elimu (Equip-Tanzania) imewekeza katika maendeleo ya
sekta hiyo.Huu ni mpango unaotekelezwa na Serikali ili
kuboresha mazingira ya mwanafunzi katika kujifunza ambao kwa sasa upo
katika mikoa mitano ikiwemo Shinyanga, Tabora, Dodoma, Simiyu na Kigoma.
Itakumbukwa Equip-Tanzania ilianzishwa kwa malengo ya kutoa
mafunzo na utendaji kazi kwa walimu pamoja na uongozi wa shule ambao
tunashuhudia unavyoendelea kutekelezwa kupitia kwa walimu wakuu.
Pia inalenga kutekeleza mipango ya usimamizi wa elimu katika
ngazi ya wilaya na mkoa kupitia kwa maofisa wake wa elimu ambao
wanasimamia ngazi za chini yake zikiwemo kata.Mpango huo
unalenga kuhakikisha kuwa ukusanyaji wa taarifa mbalimbali, takwimu na
uwajibikaji katika suala zima la elmu mashuleni unafanyika ili kuboresha
sekta hiyo.
Lengo lingine la mpango huo ni ushirikishwaji wa jamii wa
moja kwa moja katika masuala ya uchangiaji wa elimu katika miradi
mbalimbali mashuleni ambayo inaendelea kutekelezwa.Hivyo
Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu katika Mkoa wa Shinyanga ni miongoni
mwa wanufaika wakubwa wa mpango huo wa kuboresha sekta yake ya elimu.
Ni dhahiri mpango huu unafanya kazi na uongozi wa mkoa na
wilaya ili kuleta ufanisi na tija katika shule na pia kuimarisha mifumo
inayozalisha shule. Kwa kifupi inasogeza rasilimali zaidi darasani na
kuhakikisha zinatumika kama ilivyokusudiwa.Ushirikishaji wananchi Kwa
vile shule zinategemea jamii ndiyo maana mpango huu unafanya kazi na
asasi za kijamii kuelimisha jamii umuhimu wa elimu na uendeshaji wa
shule hizo.
Ushirikiano huu unawafanya wazazi waweze kuona shule
zinavyofanya kazi, jamii kupata taarifa sahihi za mapato na matumizi ya
fedha za shule na hivyo waweze kutoa maoni ili kusaidia kuziboresha.Tukitupia
macho namna ambavyo wazazi katika shule ya msingi Mhunze kata ya
Kishapu tunaona namna ambavyo walivyoweza kutumia nguvu kazi zao katika
ujenzi wa vyoo vya wanafunzi.Awali wakati wa changamoto
hiyo kulisababisha uharibifu mkubwa wa mazingira na harufu mbaya maeneo
ya shule kutokana na wanafunzi kujisaidia vichakani.
Pia muda wa mapumziko ulikuwa mrefu tofauti na ilivyo kawaida
ili kuwawezesha kupata muda wa kujisaidia huku wengine wakirudi
majumbani kwa ajili hiyo.Aidha pamoja na hayo lakini pia
kwa baadhi ya wanafunzi ilikuwa ikiwaathiri kisaikolojia ambapo
wanafunzi hao waliona shule si sehemu salama tena kwa mustakabali wa
afya zao.
Hivyo wanafunzi hao walikacha shule na hivyo kusababisha hali
ya utoro huku wengine wakishindwa kuzingatia masomo wanayofundishwa
hivyo kuchangia kushuka kwa taaluma.Hatua zilizochukuliwa Kutokana
na hali hiyo, Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kupitia idara zake za
Mipango na ile ya Elimu Msingi zimekuja na mkakati wa kuhakikisha
changamoto hiyo inatatuliwa.
Mchumi kutoka Ofisa Mipango Kishapu, Noela Levira anasema
kuwa halmashauri inatekeleza miradi mbalimbali ya elimu kwa kushirikisha
nguvu za wananchi.Anasema kuwa wananchi wanapokusanya
nguvu zao na kujenga japo maboma ya majengo mfano madarasa, nyumba za
walimu au vyoo wanapofikia hatua hiyo Serikali inamalizia kujenga.
Kama ilivyo mojawapo ya malengo ya mpango huo yaani
ushirikishwaji wa wananchi, shule hiyo iliitisha kikao cha wananchi
kujadili kuhusu utatuzi wa changamoto hiyo.Hivyo wananchi
hao wakiwemo wazazi kwa umoja wao waliazimia kuchangia nguvu kazi katika
kutekeleza mradi wa ujenzi wa vyoo kwa ajili ya wanafunzi hao.Jitihada
hizo zimesaidia ukamilishaji wa jumla ya matundu 15 ya vyoo yamejengwa
ambapo kati yake manane kwa ajili ya wasichana na saba ya wavulana.
Pia Uwiano wa wanafunzi na matumizi ya vyoo kwa wanafunzi
umekuwa wa wastani na hivyo kumpa kila mmoja nafasi ya kujisitiri
tofauti na ilivyokuwa zamani.Kutokana na uborekaji huo wa
miundombinu ya vyoo shuleni mahudhurio ya wanafunzi yameongezeka kutoka
asilimia 80 ya awali hadi kufikia asilimia 95 hivyo taaluma kupanda.Wadau wanazungumzia hali ya kuchangia elimu?
Mwakilishi wa wananchi, Isaka Maige anasema wazo la wazazi na
wananchi kwa ujumla kuchangia nguvu kazi katika suala la elimu ni zuri
na limekuwa na tija.Anatolea mfano wazo la kushirikisha
wananchi katika ujenzi wa matundu ya vyoo lilipokelewa kwenye vikao na
kutekelezwa ingawa kulikuwa na changamoto chache.
Anasema baadhi ya wananchi walikacha kuchangia na wengine
wakidai kamati ya shule inatumia fedha bila kuzifanyia kazi inayopaswa
kufanyika katika utekelezaji miradi.Hata hivyo, mzozo huo ulitatuliwa baada ya kamati hiyo kuonesha orodha na idadi ya wachangiaji na fedha zilizopatikana.
Ni dhahiri kuwa mafanikio katika shule zetu nchini yanayaweza
kuchangiwa na ushirikishaji wa jamii na wadau mbalimbali na si tu
kusubiri kila kitu kifanywe na Serikali. Pia elimu ya
darasani pekee haitoshi kumpatia mtoto ufaulu mzuri bali na afya yake
ikiwa ni pamoja na mazingira yaimarike shuleni na nyumbani.
COMMENTS