Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limetoa ujumbe wa Kwaresma wa mwaka 2018 ndani yake likitoa msimamo kuhusu masuala ya kisias...
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania
(TEC) limetoa ujumbe wa Kwaresma wa mwaka 2018 ndani yake likitoa
msimamo kuhusu masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii nchini.
Ujumbe huo ulioandikwa na maaskofu wote
36 wa TEC wakiongozwa na Rais wake, Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa upo
katika kitabu cha kurasa 20 ikiwa ni maandalizi ya ibada hiyo ya siku
40, kipindi ambacho ni cha mfungo wa sala kukumbuka siku 40 za Kristo
kufunga na kwenda jangwani.
Hali ya kisiasa
Katika ujumbe huo, TEC imesema uamuzi wa
Serikali kuzuia maandamano, mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa ni
kwenda kinyume cha Katiba ya nchi.
Baraza hilo pia limeonya hatua ya Serikali kuvibana vyombo vya habari ikiwa pamoja na kuvifungia kwa sababu mbalimbali.
“Kufungiwa huku kwa vyombo vya habari
kumeenda sambamba na kuminya uhuru wa Mahakama na Bunge kwa njia ya
kuminya haki wabunge na kutowapa nafasi ya mikutano ya hadhara kama haki
yao ya msingi ya kikatiba.”
“Kikatiba, nchi yetu inafuata mfumo wa
demokrasia ya vyama vingi. Katiba na sheria mbalimbali zimeainisha
utaratibu wa kazi na shughuli za vyama vya siasa. Ili kuhakikisha kwamba
shughuli za vyama vya siasa zinakuwa endelevu, vyama vyenye kukidhi
vigezo hupewa ruzuku kupitia bajeti ya Serikali inayopitishwa na Bunge,”
unaeleza ujumbe huo.
“Hata hivyo, shughuli za, siasa bado
zinaendelea kuzuiwa kwa kutumia vyombo vya dola. Maana yake ni kwamba
shughuli za kiuenezi za vyama vya siasa, kama vile mikutano ya hadhara,
maandamano, makongamano, mijadala na hata mikutano ya ndani, ambayo ni
haki ya kila raia, zimekoma mpaka uchaguzi mwingine. Kisheria, huu ni
uvunjifu wa Katiba na sheria za nchi.”
Kuhusu vyombo vya habari, TEC imesema
Serikali imepunguza wigo wa uhuru wa wananchi wa kupata habari na maoni
ya kujieleza na kueleza kwamba kwa ujumla wake, mazingira hayo
yatasababisha jamii kufarakana na hata kujenga chuki.
“Kumekuwapo pia hali ya vurugu katika
chaguzi mbalimbali. Chaguzi hizi zinaacha nyuma uchungu, hasira, tamaa
ya kulipa kisasi na hata kususia chaguzi nyingine,” unasema ujumbe huo
wa TEC na kuonya kuwa kama hali hiyo itaachwa, itakuja kusababisha
mifarakano mikubwa itakayobomoa amani na umoja wa kitaifa.
Kuhusu uchumi, TEC imetoa mambo sita ya
kujiuliza; “Tunazitumiaje mali na rasilimali nyingine tulizokabidhiwa na
Mungu kama mawakili wake? Tunalipa kodi stahiki kwa ajili ya kugharamia
huduma za jamii ambazo Serikali inapaswa kutoa kwa ajili ya wananchi?”
“Wale ambao tu waajiri, tunawajali
wafanyakazi na wahudumu wetu kwa kuwalipa mishahara ya halali? Wale
ambao tu wafanya biashara, tunalipa kodi zote kihalali?”
“Wale ambao tumepewa jukumu la kukusanya
kodi, ushuru na ada nyingine kama tunafanya hivyo kwa mujibu wa sheria,
kanuni na taratibu husika? Tunaepukaje na kishawishi cha rushwa, hongo,
mulungula, magendo au aina yoyote ya ufisadi?”
Katika eneo la kijamii TEC imesema bado kuna kishawishi cha kupingana na azma ya kuboresha maisha ya kijamii.
“Hii inajidhihirisha kwa njia ya
uhasama, ugomvi, ukatili kwa watoto na wanawake, ujambazi, na maovu
mengine kama hayo miongoni mwa jamii yetu. Kama wamisionari tunaopaswa
kuleta habari njema kwa ndugu zetu, kwa nini turuhusu roho ya namna hii
ambayo kwa kweli ni roho ya Kaini inayouliza kwa jeuri kabisa,” unasema
ujumbe huo.
Katika ujumbe wake, Baraza hilo
limesema, “Kwa mwaka huu wa 2018 kipindi hiki ni cha kujitafakari mbele
ya Mungu na kufanya toba hususan uhai wa amani yetu kwa njia ya matendo
ya huruma, haki upendo na amani kwa jirani zetu.”
Limesema hiki ni kipindi chenye upekee wa aina yake kwake sababu ya mambo matatu;
“Ni katika mwaka huu ambapo Kanisa
Katoliki Tanzania linaadhimisha na kusherehekea miaka 150 ya Ukatoliki
Tanzania Bara, na kilele chake kitakuwa tarehe 2 Oktoba.
Mwaka huu pia utakuwa ni mwaka wa 50
tangu Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania watoe tamko rasmi kuhusu
mwelekeo na hatima ya nchi yetu na Mwaka huu ni mwaka wa maandalizi ya
utekelezaji wa haki ya msingi ya kidemokrasia ya raia wote ya kuchagua
viongozi wa Serikali zetu za mitaa, vijiji na vitongoji hapo mwakani
2019.”
Kwa sababu hizo tatu, TEC imesema, “Ni
vyema tafakari yetu ya Kwaresima ikalenga katika swali ambalo, kwa namna
moja au nyingine, linahusu sababu hizo tatu. Kwa njia ya swali hilo
mwanadamu hudiriki kumhoji na kumuuliza Mungu na Muumba wake kuhusu hali
ya binadamu mwenzake. Swali hilo ni Je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?”
(Mw. 4:9).
SOMA WARAKA WOTE HAPA CHINI
Basi enendeni,
mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu ndiyo kauli mbiu
inayoongoza ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa mwaka
2018. Ni ujumbe unaozingatia matukio makuu matatu: Jubilei ya Miaka 150
ya Ukristo Tanzania Bara, Miaka 50 ya Tamko la Maaskofu kuhusu Mwelekeo
na Hatima ya Tanzania na Maandalizi ya Uchaguzi wa viongozi wa Serikali
za mitaa utakaofanyika mwaka 2019. Wapendwa Familia ya Mungu, Na Watu
Wote wenye Mapenzi Mema, “Neema na iwe kwenu, na amani zitokazo kwa Mungu, Baba yetu” (Kol 1:2).
Utangulizi
Kama
ilivyo ada ya Wakristo pote ulimwenguni, kwa kipindi cha siku arobaini
kabla ya kuadhimisha Jumapili ya Ufufuko wa Bwana Wetu Yesu Kristo,
Wakristo hutumia muda huo kufunga, kufanya toba na kufanya matendo ya
huruma kwa wote wenye mahitaji huku wakijitafakari kuhusu uhalisia wa
hali yao ya kuwa ni wenye dhambi mbele ya Mungu, ili waweze kufanya toba
ya kweli na yenye mageuzi na wongofu katika maisha. Mwaka huu kipindi
hiki, kijulikanacho kama kipindi cha Kwaresima, kinaanzia tarehe 14
Februari Jumatano, siku ambayo inajulikana kwa jina la Jumatano ya
Majivu, mpaka tarehe 29 Machi, ambayo itakuwa ni siku ya Alhamisi Kuu.
Kwa
mwaka huu wa 2018 kipindi hiki, cha kujitafakari mbele ya Mungu na
kufanya toba hususan uhai wa imani yetu kwa njia ya matendo ya huruma,
haki, upendo na amani kwa jirani zetu, ni kipindi chenye upekee wa aina
yake kwa sababu kuu tatu: 1) Ni katika mwaka huu ambapo Kanisa Katoliki
Tanzania linaadhimisha na kusherehekea miaka 150 ya Ukatoliki Tanzania
Bara, na kilele chake kitakuwa tarehe 2 Oktoba; 2) Mwaka huu pia utakuwa
ni mwaka wa 50 tangu Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania watoe tamko
rasmi kuhusu mwelekeo na hatima ya nchi yetu; na 3) Mwaka huu ni mwaka
wa maandalizi ya utekelezaji wa haki ya msingi ya kidemokrasia ya raia
wote ya kuchagua viongozi wa serikali zetu za mitaa, vijiji na
vitongoji hapo mwakani 2019. Kwa sababu kuu hizo tatu, ni vema tafakari
yetu ya Kwaresima ikalenga katika swali ambalo, kwa namna moja au
nyingine, linahusu sababu hizo tatu. Kwa njia ya swali hilo mwanadamu
hudiriki kumhoji na kumuuliza Mungu na Muumba wake kuhusu hali ya
binadamu mwenzake. Swali hilo ni “Je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?”
(Mw. 4:9).
Hali
halisi ya nchi yetu, kwa yeyote anayesoma ishara za nyakati kwa makini,
inalifanya swali hilo liwe na uzito wake kuendana na sababu hizo kuu
tatu zilizotolewa. Lakini pia, tukumbuke kuwa mwaka 2018 ni mwaka wa
sabini (70) tangu Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa walipotamka rasmi
na kujifunga kuhakikisha kuwa Tamko la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu la
mwaka 1948 linatekelezwa. Na sasa tuone ni kwa namna gani swali hilo
linatuhusu kwa kuangalia misingi ya sababu hizo kuu tatu.
Kuhusu sababu ya kwanza,
ni lazima tunapoadhimisha miaka 150 ya Ukatoliki Tanzania Bara
tujiulize hilo swali kwa namna ifuatayo: “Je, sisi Wakatoliki katika
kipindi hicho cha miaka 150 tumekuwa walinzi wa binadamu wenzetu, ambao
tumefanywa kuwa ndugu zao kama Familia ya Mungu kupitia Mwanae Yesu
Kristo na Mama yetu Bikira Maria?”. Kuhusu sababu ya pili,
tujiulize swali hilo hilo kama ifuatavyo: “Je, katika kipindi hicho cha
miaka hamsini, kuanzia 1968 mpaka mwaka huu 2018, sisi Wakatoliki
tumekuza roho na moyo wa kuwajali binadamu kama ndugu zetu, kuendana na
barua ya kichungaji ya mwaka huo, yenye kichwa cha habari The Church and Developing Society of Tanzania, iliyotuasa
kuwa falsafa na imani ya Azimio la Arusha, Azimio ambalo lilitoa
mwelekeo na hatima ya nchi yetu, inakubaliana kwa karibu kabisa na ( kwa
kunukuu sehemu ya ujumbe huo) “roho ya kweli ya Kristo na Kanisa, roho
ambayo ni ya udugu, ya kumegeana, ya kuhudumiana na ya kufanya kazi kwa
bidii?” Kwa kusisitiza ukaribu huo kati ya Azimio la Arusha na roho ya
kweli ya Kikristo, barua hiyo ya kichungaji ilizingatia barua ya Yakobo,
2:14-17 inayosema kuwa imani bila matendo ni imani mfu!
Kuhusu sababu ya tatu,
baada ya kufanya toba na kusherehekea Ufufuko wa Bwana Wetu Yesu
Kristo, tukiwa na ari na mwelekeo mpya wa maisha ya Kikristo
yanayodhirishwa na imani hai, swali hilo tulihusishe na dhamira ya kweli
ya viongozi wetu watarajiwa wa serikali za mitaa, kwa kujiuliza, “Mwaka
huu wa maandalizi ya kuchagua viongozi wa serikali zetu za mitaa,
vijiji na vitongoji, tufanye nini ili maandalizi yetu ya uchaguzi yatupe
viongozi wetu wa karibu ambao hawatakwepa wajibu wao kwa kujitetea kwa
mtazamo wa swali kama hilo?” Hivyo basi, ili kuhakisha kuwa tuna pata
majibu ya kweli na yenye kuleta mabadiliko katika nafsi zetu na
mahusiano na mashirikiano katika jamii yetu, ujumbe huu wa Kwaresima una
lengo la kuwahimiza, kuwahamasisha na hata kuwadai waumini Wakatoliki
wote kuuitikia kwa moyo wa toba, mageuzi na kushiriki kwa kujitoa zaidi
katika uinjilishaji wa nchi yetu kama mwanga na chumvi ya ulimwengu wa
Tanzania.
Kufikia
lengo hilo, tunahimiza Jumuiya Ndogondogo katika kila parokia
ziutafakari kwa makini ujumbe huu, zipange namna ya kuutekeleza kwa
kuzingatia hayo maswali matatu. Ili kufanikisha hilo, tunatoa mwongozo
ufuatao katika hatua tatu: 1) Kusoma ishara za nyakati za Tanzania na
kuzichambua; 2) Kuzitathmini ishara hizo kwa misingi ya Injili na tunu
za Ufalme wa Mungu kuendana na masomo na Injili ya Jumatano ya Majivu;
na 3) Kufanya maamuzi yatokanayo na tathmini hiyo na kupanga utekelezaji
wa maamuzi hayo. Tunawaalika basi, tutembee pamoja katika kulitafakari
fumbo la imani yetu, huku tukiomba neema ya Mungu ifanye kazi ndani yetu
na kutujalia kukua katika kumpenda, kumjua na kumtumikia Mungu na vivyo
hivyo kumpenda jirani huku tukitumikiana sisi kwa sisi.
SURA YA KWANZA: BASI ENENDENI
Wamisionari
waliokuja kuinjilisha Tanzania ya sasa walifika Zanzibar mwaka 1860
wakitokea jimbo la Reunion. Miaka minane baadae, Wamisionari wa Shirika
la Roho Mtakatifu, wakisukumwa na shauku ya kuinjilisha maeneo mapana
zaidi, walisafiri kutoka Zanzibar na kutia nanga katika mji wa Bagamoyo
mnamo mwaka 1868, ambapo walianzisha jumuiya ya kwanza ya wakristo ambao
wengi wao wakiwa ni wale waliokombolewa kutoka utumwani. Hivi jumuiya
hii ya kwanza ya Wakristo ikawa na sifa ya kukombolewa, si tu kiimani,
bali hata kijamii. Hawa walifanywa kuwa watu huru kiroho, kimwili na
kiutu. Mwanzo huu wa imani Zanzibar na Bagamoyo umekuwa mlango wa imani
kwa maeneo yote ya ukanda huu wa Maziwa Makuu. Kwa upande wao,
Wamisionari wa Afrika wlijielekeza maeneo ya Magaharibi ya Tanganyika na
kuvuka maziwa yote makuu. Nao Wamisionari Wabenediktini, baadaye,
walielekea maeneo ya Kusini mwa Tanganyika. Makundi haya matatu
yalifuatiwa na wamisionari wa Mashirika mengine waliosambaa maeneo
mbalimbali ya tanganyika.
Roho ya umisionari
Kanisa
kwa asili yake ni la kimisionari. Umisionari ndiyo mtima wa Kanisa, na
mmisionari hajitumi bali anatumwa. Mmisionari wa kwanza ni Bwana Wetu
Yesu Kristo. “Kama vile Baba alivyonituma mimi, nami nawatuma ninyi” (Yn
20:21). Kisha wale wote waliomvaa Kristo kwa Ubatizo nao kwa muda wao,
hali zao na mazingira yao wanatumwa kuendeleza utume wa Kristo.
Wanatumwa kuujenga Ufalme wa Mungu. Anayetumwa hapeleki ujumbe wake,
haendi kujihubiri mwenyewe, bali anapeleka ujumbe wa yule anayemtuma.
Ujumbe unaobeba utume wetu uko wazi: “Enendeni basi, mkawafanye watu wa
mataifa yote wawe wanafunzi wangu” (Mt 28:19). Sisi tulimpokea Kristo
na kufanyika kuwa wanafunzi wake tunatumwa kuwafanya mataifa yote pia
kuwa wanafunzi wake. Bwana Yesu anayetutuma anatuelekeza ni kwa namna
gani tunaweza kuutekeleza wajibu na utume huo mkubwa: “Mkiwabatiza kwa
jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu. Wafundisheni kuyashika
maagizo yote niliyowapeni” (Mt 28:19b-20).
Sadaka ya umisionari
Umisionari
ni kutoka: “Enendeni basi”. Bwana wetu Yesu Kristo hakuwaambia mitume
wake wakae wangojee watu waje. Hapana. Tokeni mkakutane wa watu
walipo. Tendo la kutoka katika mazingira tuliyozoea, hali, maisha na
usalama tulionao inadai kuwa tayari kutoa sadaka. Wamisionari waliokuja
kwetu waliacha yote: jamaa, mali, usalama, raha, n.k.; wakaja
kukabiliana na adha, magonjwa, hatari na hata kifo kilichotokana na
maradhi ya nchi za ukanda wa joto (tropikali), kushambuliwa na wanyama
na hata kushambuliwa na maharamia. Walitoa sadaka kubwa.
Na
jambo kubwa ni kwamba walitoa sadaka hiyo kwa furaha. Ari na kiu yao
ilikuwa kutekeleza agizo la Kristo: “Enendeni basi”. Walitamani kufika
hata miisho ya dunia ili kuwafanya watu wamjue, wampende na wamtumikie
Mungu na hivi kufanyika kuwa wanafunzi wake. Ndiyo maana hata pale
ambapo wengi wao walipofariki kutokana na adha tulizoona hapo juu, bado
wengine walikuja tu kwa furaha bila woga. Kwani katika kujitoa maisha
yao kama sadaka walipata faraja ya ahadi ya Kristo kwa wale wote
wanaoitikia mwito wa “Enendeni basi!”. Wamisionari hao waliifahamu
ahadi ya Kristo na ndiyo maana hiyo ilikuwa faraja yao. Petro
anapomwuliza Yesu, “Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata tutapata
nini basi?” (Mt 19:27). Yesu anamjibu akitoa ahadi bora kabisa:
Aliyeacha vyote kwa ajili ya jina lake, “atapokea mara mia, na kuurithi
uzima wa milele” (Mt. 19:29). Bwana Yesu anapowatuma wanafunzi wake
alipokuwa anakaribia kupaa Mbinguni, aliwaambia, "… enendeni ulimwenguni
mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa Jina la Baba na
la Mwana na la Roho Mtakatifu, nanyi wafundisheni kuyashika mambo yote
niliyowaamuru ninyi. Hakika Mimi niko pamoja nanyi sikuzote, hadi mwisho
wa nyakati. Amen” (Mathayo 28:19-20).
Maneno
haya ya Yesu yanaonesha upendo wa hali ya juu aliokuwa nao Mungu kwa
wanadamu, kutupa nafasi ya kuwa wana wa Mungu. Kumfahamu Mungu kwa
kuacha njia zetu mbaya. Yesu hakuwaambia wanafunzi wake wasubiri watu
wawafuate, ili wapate kuwafundisha na kuwabatiza, lakini aliwaambia
wawafuate watu walipo, na kuwafundisha juu ya Ufalme wa Mungu na
kuwabatiza katika Utatu Mtakatifu, yaani Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.
Maagizo haya ya Yesu yalifuatwa na kwa sababu hiyo watu wote duniani
tumepata kumjua Mungu wa kweli kupitia kwa Mwanae. Bahati kubwa namna
gani! Yesu anatutaka wote tupate kuwa wamisionari kwa wenzetu, kwani
ijapokuwa tumepata kumjua Mungu, na kuwa wakristo, yafaa kujiuliza ni
mara ngapi tunamuishi Kristo? Ni mara ngapi tunaonekana kwa watu wengine
wasiomjua Kristo bado kuwa sisi tu wana wa Mungu kwa pendo la kuitwa
wana wa Mungu? (1 Yoh 3:1).
Mtakatifu
Yohane Mwinjili katika Waraka wake wa kwanza kwa watu wote anasema:
“Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa;
lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana
tutamwona kama alivyo. Na kila mwenye matumaini haya katika yeye
hujitakasa, kama yeye alivyo mtakatifu” (1Yoh 3:2-3). Ni dhahiri kila
mmoja wetu anatamani na kuweka tumaini lake katika kumuona Mungu. Lakini
je, mara ngapi tunamwona Mungu kupitia ndugu zetu na wale
wanaotuzunguka? Je, kumuona Mungu ni Kanisani tu au hata kwenye jamii?
Haya ni maswali ambayo kila mmoja wetu anapaswa kujiuliza. Kazi
alizotupa Mungu ni kwa ajili ya utukufu wake. Kazi ni huduma, kwa maana
unafanya kazi unayofanya ili kumsaidia mtu mwingine. Je, huyo
unayemsaidia anaonja upendo wa Kristo ndani yako? Anapata kumsifu na
kumshukuru Mungu kupitia wewe? Kama jibu ni hapana, basi yafaa
kujitafakari kwa upya.
Umisionari
ni zawadi, ni sadaka ni upendo unaozidi hali yetu ya kibinadamu. Ni
kule kumpendeza Mungu na kutamani kila anayekuzunguka aonje pendo la
Mungu. Umisionari wa sasa si kama ule uliokuwa miaka 150 iliyopita,
ambapo kuinjilisha ilikuwa ni muhimu na lazima kwani watu hawakuwa
wakimjua Mungu wa kweli. Unijilishaji ulifanikiwa, ijapokuwa kwa
kukabiliana na changamoto nyingi, kwa ajili ya upendo na ujasiri wa
kimungu wamisionari hawa waliokuwa nao. Uinjilishaji mpya leo hii
unalenga kuwasaidia Wakristo kuuishi Ukristo kadiri ya mazingira ya leo,
na kufanya hivyo kwa matendo, na hivyo kuwa kielelezo cha kweli cha
imani.
SURA YA PILI: SASA NI ZAMU YETU
Mwenyeheri
Paulo VI alipotembelea Uganda mwaka 1969 alilikumbusha Kanisa katika
Afrika kwamba wakati umewadia wa kuwa wamisionari baina na miongoni
mwetu. Akisemea jambo hilo nchini Uganda, Paulo VI alisema: “Kwa sasa,
ninyi Waafrika mu wamisionari baina na miongoni mwenu. Kanisa la Kristo
limekwisha pandwa vema na kwa uhakika katika udongo huu uliobarikiwa.
... Kwa maneno mengine, ninyi Waafrika lazima sasa, katika Bara hili,
muendeleze ujenzi wa Kanisa.... Kanisa kwa maumbile yake daima ni Kanisa la kimisionari”. Hii
ni kutaka kusema kwamba hatupaswi kudhani kuwa mmisionari ni mtu
anayetoka nje ya nchi kuja kwetu. Umisionari kwa maana pana ni
kumshuhudia Kristo kwa maneno na matendo yetu popote tulipo. Umisionari
ni kuachana na ubinafsi, ni kukumbuka kuwa popote tulipo tunapaswa
kutenda na kunena yale yanayojenga Ufalme wa Mungu na kusaidia kuwafanya
watu wengi kuwa wanafunzi wa Kristo. Kristo anaposema, “Nanyi mtakuwa
mashahidi wangu” (Mdo 1:8), anataka kusema kama tumemsikia, kama
tumemjua, na zaidi sana kama tunampenda, basi hatuwezi kuacha
kumshuhudia kwa wengine. Moto wa furaha wa kumjua Kristo utatusukuma
kuhakikisha tunafanya kila tunavyoweza ili mwana wa mtu atakapokuja
akute bado kuna imani duniani (Rej. Lk 18:8).
Jambo
hili linadai ujasiri wa imani utokao kwa Roho Mtakatifu. Ndiyo maana
Mitume wa Yesu hata walipokamatwa, kuteswa na kufungwa hawakurudi nyuma:
“Hatuwezi kuacha kusema juu ya mambo yale tuliyoyaona na kuyasikia”
(Mdo 4:20). Baba Mtakatifu Francisko, katika hati yake ya kichungaji
Furaha ya Injili (Evangelii Gaudium, 14), anapendekeza mambo haya yafuatayo yatubidishe:
1. Kuwasaidia waamini wakue kiroho ili waweze kupokea upendo wa Mungu kwa utimilifu zaidi katika maisha yao.
2. Kuwasaidia
wabatizwa ambao maisha yao hayaonyeshi wajibu wa ubatizo, ambao hawana
uhusiano wa maana na Kanisa na hawapati tena faraja inayotokana na
imani.
3. Umuhimu wa kuihubiri Injili kwa wale ambao bado hawamtambui Yesu Kristo au daima wamemkataa.
Hii ndiyo namna bora
kabisa ya kuwa “katika hali ya umisionari daima” (EG, 25), na ndiyo
namna ya kudhirisha kuwa sasa ni zamu yetu nasi kuhubiri yale tuliosikia
na kuyaona. Bidii ya kufanya mambo hayo matatu yaliyotajwa na Baba
Mtakatifu Fransisko itatuepusha na tabia ya Kaini ambaye hakujali wala
hakuona kuwajibika juu ya mustakabari wa ndugu yake Abeli. Hivyo basi,
kuwa mmisionari kunahitaji sana moyo wa kujali kabisa hatima ya wokovu
ya kila binadamu kwa kumjali katika nyanja zote za maisha yake kiroho,
kiakili, kimwili na kijamii. Bila ya kuwa na moyo wa kujali, tutakuwa
wakatili kama Kaini alivyokuwa kwa ndugu yake Abeli!
SURA YA TATU: “MIMI NI MLINZI WA NDUGU YANGU?”
Moja
ya majibu ya kukatisha tamaa kabisa katika Maandiko Matakatifu ni hili
jibu la Kaini anapoulizwa na Mungu baada ya kuwa amemwua ndugu yake
Abeli, “Yuko wapi Abeli ndugu yako?” (Mwa 1:9), Kaini anajibu, “Sijui,
mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?” (Mwa 4:9b). Kaini hajali na haoni
kuwajibika kwa namna yoyote juu ya mustakabari wa ndugu yake. Lakini
zaidi sana, anakuwa ni kielelezo cha dhamiri iliyokufa, kwani anajua
kilichotokea na hajali lolote kuhusu hali ya ndugu yake! Ni kwa
mtazamo huo basi nasi tujitathmini na tuwe wa kweli kwa dhamiri zetu.
Je, kama wamisionari tunaowajibika kwa ndugu zetu, tunaelezaje hali
ilivyo sasa katika jamii yetu ya Tanzania? Je, tunasoma alama za nyakati
zetu vema kiasi kwamba tunaguswa kama wamisionari na tunapeleka Habari
Njema inayoonesha kuwa sisi ni walinzi wa ndugu zetu?
Dalili za Nyakati Zetu Tanzania
Ili
kuweza kuleta mabadiliko katika nafsi zetu na katika jamii yetu, Kanisa
siku zote linatufundisha, kwa busara na hekima ya Roho wa Mungu,
ulazima wa kusoma ishara za nyakati ili kujua ni nini kinachoendelea
katika jamii. Kuhusu nchi yetu ishara za nyakati tutaziangalia katika
maeneo matatu, yaani kisiasa, kijamii na kiuchumi, kwa lengo la
kujitathimini.
- Kisiasa Kikatiba, nchi yetu inafuata mfumo wa demokrasia ya vyama vingi. Katiba na Sheria mbalimbali zimeainisha utaratibu wa kazi na shughuli za vyama vya siasa. Ili kuhakikisha kwamba kazi na shughuli za vyama vya siasa zinakuwa endelevu, vyama vyenye kukidhi vigezo hupewa ruzuku kupitia Bajeti ya Serikali inayopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania. Hata hivyo, shughuli za siasa bado zinaendelea kuzuiwa kwa kutumia vyombo vya dola. Maana yake ni kwamba shughuli za kiuenezi za vyama vya siasa, kama vile mikutano ya hadhara, maandamano, makongamano, mijadala na hata mikutano ya ndani, ambayo ni haki ya kila raia, zimekoma mpaka uchaguzi mwingine. Kisheria, huu ni uvunjifu wa Katiba na Sheria za nchi.
Vile vile baadhi ya
vyombo vya habari vimefungiwa au kusimamishwa kwa muda, na hivyo
kupunguza uwigo wa uhuru wa wananchi wa kupata habari, maoni na wa
kujieleza. Kufungiwa huku kwa vyombo vya habari kumeenda sambamba na
kuminya uhuru wa Mahakama na Bunge kwa njia ya kuminya haki ya wabunge
na kutowapa nafasi ya mikutano ya hadhara kama haki yao ya msingi ya
Kikatiba. Katika mazingira haya ni rahisi kwa jamii kufarakana na hata
kujenga chuki kiasi cha kuhatarisha amani, usalama na hadhi ya uhai wa
binadamu. Kumekuwapo pia hali ya vurugu katika chaguzi mbalimbali.
Chaguzi hizi zinaacha nyuma uchungu, hasira, tamaa ya kulipa kisasi na
hata kususia chaguzi nyingine. Hali hii ni hatari kwa mustakabali wa
Taifa letu. Tukiiachia hali hii izoeleke tushishangae huko mbeleni
kujikuta katika mifarakano mikubwa zaidi itakayobomoa misingi ya amani
na umoja wa kitaifa.
- Kiuchumi Hapa ni vema tukajiuliza maswali ya msingi kabisa kuhusu kujali katika maisha ya walio wanyonge ili umisionari wetu ulete nafuu katika mahitaji ya lazima kwa wale wanyonge, maskini na walio pembezoni mwa jamii. Hebu tujiulize:
- Tunazitumuaje mali na rasilimali nyingine tulizokabidhiwa na Mungu kama mawakili wake?
- Tunalipa kodi stahiki kwa ajili ya kugharamia huduma za jamii ambazo serikali inapaswa kutoa kwa ajili ya wananchi?
- Wale ambao tu waajiri, tunawajali wafanyakazi na wahudumu wetu kwa kuwalipa mishahara ya halali?
- Wale ambao tu wafanya biashara, tunalipa kodi zote kihalali?
- Wale ambao tumepewa jukumu la kukusanya kodi, ushuru na ada nyingine tunafanya hivyo kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu husika?
- Tunaepukanaje na kishawishi cha rushwa, hongo, mulungula, magendo au aina yoyote ya ufisadi?
- Kijamii
Sasa hivi bado kuna
kishawishi cha kupingana na azma ya kuboresha maisha ya kijamii. Hii
inajidhihirisha kwa njia ya uhasama, ugomvi, ukatili kwa watoto na
wanawake, ujambazi, na maovu mengine kiama hayo miongoni mwa jamii yetu.
Kama wamisionari tunaopaswa kuleta habari njema kwa ndugu zetu, kwa
nini turuhusu roho ya namna hii ambayo kwa kweli ni roho ya Kaini
inayouliza kwa jeuri kabisa: ‘Mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?’
SURA YA NNE: NIMRUDISHIE BWANA NINI?
Alama za nyakati katika jamii yetu ya leo, na tafakari kuhusu maswali
yaliyoulizwa havina budi kutupa msukumo ambao ni kinyume kabisa na
mtazamo wa Kaini. Msukumo huo ni ule unaoanzishwa na kutambua mema
aliyotufanyia Mungu Baba, hasa lile jema kuu la kuletewa, kuikubali na
kuiishi Injili ya Bwana Wetu Yesu Kristo kama wamisionari wake
waaminifu. Na moyo huu unasimama juu ya swali “Nimrudishie nini Bwana
kwa mema aliyonitendea?” (Zab. 116:12) Neno la Bwana Mungu wetu na Baba
wa Mkombozi wetu Yesu Kristo, kama linavyosomwa siku ya Jumatano ya
Majivu, siku tunapoanza kipindi cha Kwarezima, lina msukumo huohuo!
Masomo pamoja na Injili ya siku hiyo yanalenga katika kukabiliana na
swali hilo la Kaini linalotuhangaisha kila siku! Hivyo ili kuonesha
shukrani kwa moyo wa kimisionari kwa Mungu Baba, ni vema tukafanya
maamuzi ya kubadilisha maisha yetu katika Kwaresima wa mwaka huu 2018.
Masomo hayo yana na dhamira husika kuu kama ifuatavyo:
- Toba ya kumrudia Mungu ni kwa njia ya kuondoa aina yoyote ya uonevu na kutenda haki
- Kukiri kuwa tu wakosefu, na tunahitaji kufanya toba.
- Kupatanishwa na Mungu kama watumishi wake ni kuwa tayari kwa lolote hata kama ni kuchekwa au kuhangaishwa na ulimwengu
- Sala, kufunga na kutoa sadaka vifanyike bila ‘kujipigia debe’!
Maamuzi na Utekelezaji ngazi ya Parokia na Jumuiya
Hivyo basi katika kujibu swali ‘Nimrudishie nini Bwana?’, maswali yafuatayo yanapendekeza kitu gani kifanyike:
4.1 Neno la Mungu linasema nini kwa Jumuiya na Parokia yetu kuhusu:
- Toba na thamani ya uhai wa watoto wetu, vijana wetu na familia zetu?
- Toba na haki za binadamu katika mila, desturi, siasa, sheria na uchumi?
- Kama wadhambi tuna wajibu gani mbele ya Mungu na mbele ya binadamu wenzetu?
4.2 Jumuiya na Parokia yetu inaweza kufanya nini ili kurekebisha na kukuza:
- Moyo na tabia ya usikivu kwa sauti ya Mungu anayetuuliza kuhusu hali ya bindamu kama ndugu zetu?
- Moyo na tabia ya kujali utu, hadhi na haki za binadamu wenzetu, hasa wanyonge na wanaogandamizwa?
- Kuchangia katika mabadiliko ya kisiasa, kijamii na kiuchumi ili maendeleo ya kweli yapatikane kadiri ya tunu za Ufalme wa Mungu?
HITIMISHO
Tukiwa tunaaadhimisha miaka 150 ya umisionari na uinjilishaji nchini
Tanzania, tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa upendo wake usiokuwa
na mpaka, si tu kwa kumtoa Mwanae wa pekee awe Mkombozi wetu, lakini pia
kwa Mwanae mpendwa kuwa sababu ya kumfahamu Mungu. Hivyo basi,
tunapofanya adhimisho hili kubwa la Kristo kati yetu, ni fursa ya
kumrudia Mungu kwa moyo wa shukrani. Sisi tulioujua upendo wa Kristo,
sisi tunaoonja katika maisha yetu nguvu na uzuri wa imani ya Kikristo
hatuna budi kumshukuru Mungu. “Nimrudishie Bwana nini kwa Ukarimu wake
wote. Nitakipokea kikombe cha wokovu na kulitangaza jina la Bwana” (Zab
116:12). Shukrani ya kweli inadhihirika katika kuwa tayari wa kukipokea
kikombe cha wokovu na kulitangaza jina la Bwana. Kwa maneno mengine,
huu ni mwaliko wa kuwa “katika hali ya umisionari daima” (EG, 25),
unaopingana kabisa na swali alilodiriki Kaini kumuuliza Mungu, ‘Mimi ni
mlinzi wa ndugu yangu?’
Tofauti kabisa na swali hilo la Kaini, ushuhuda wa imani unadai ujasiri
na unabii, kama walivyo wale wamisionari waliotuletea imani. Pale
tulipolegelega tunapaswa “tuvumbue tena upya na kuongeza shauku yetu ile
furaha ya kuinjilisha yenye kuburudisha na kufariji, hata pale ambapo
tunapaswa kupanda kwa machozi” (EG, 10).Baada ya miaka 150, uinjilishaji
bado upo na unahitajika. Wewe Mkristo, unaitikiaaje? Kwa michango na
sadaka zetu zinazofanikisha waseminari kusoma na kuwa mapadri, watawa
kupata mahitaji yao, wagonjwa kupewa neno la upendo na faraja, wafungwa
kutembelewa, mayatima na wajane kupewa haki zao. Watu kuhudumiwa vizuri
katika vituo vya kazi na huduma, hata kuiona sura ya Mungu kupitia sisi,
huo ndio uinjilishaji mpya na wa sasa. Katika kipindi hiki cha
Kwaresima, ni muhimu kutafakari ni kwa namna gani tunamuishi Kristo, na
kwa namna gani tunashindwa kumuishi Kristo na kuomba neema na msamaha
wake. Tunahitaji kutambua ya kwamba sisi sote tu wamisionari wa Kristo,
kwa wenzetu wapate kumjua kama ambavyo kwa sadaka za watu wengine sisi
nasi tulipata kumjua Yesu.
Ni
rahisi zaidi kuona kama si kitu sana kuwa Mkristo Mkatoliki kwakuwa tu
ndani na tunabahati hiyo. Hatuoni kama bahati tena wala ajabu ya upendo
wa Mungu kwetu. Lakini kuna watu wengi sana wanaotamani kumjua Kristo na
hawajapata nafasi hiyo, na wengine wanaipata ilihali jua limekwisha
kutua. Katika kipindi hiki cha Toba, tukae chini tena na kutafakari kwa
upya, ni kwa namna gani maisha yetu yanamuishi Kristo, na tudhamirie
kujirudi na kutaka kufanya mapenzi ya Mungu. Hivyo basi, Wapendwa
Familia ya Mungu, Kwa moyo wa upendo na kuwajali tunawahimiza waamini
mfanye toba ya kweli ili Mungu aguse na abadilishe mioyo yetu, ya raia
wengine na viongozi wa nchi. Tuichukulie Kwaresima ya mwaka huu (2018)
kuwa ni sehemu ya maandalizi ya adhimisho la Jubilee lenye lengo la
kujenga upya Kanisa Katoliki Tanzania na lenye wamisionari wengi
watakaoweza kutumwa popote ulimwenguni. Na, mwisho tunapenda kuwatia
moyo zaidi ili mshiriki zaidi katika katika maswala ya kisiasa,
kiuchumi, kijamii na kiutamaduni, na kwa ukristo wenu muwe chumvi na
mwanga kwa wote.
Kristo Mfufuka awape amani!
COMMENTS