Na Masanja Mabula -Pemba BAKAR Khamis (25) mkaazi wa Mitondooni Wilaya ya Wete, anadaiwa kumnajisi (kumlawiti) mtoto wa kiume mwenye...
Na Masanja Mabula -Pemba
BAKAR Khamis (25) mkaazi wa Mitondooni Wilaya ya Wete, anadaiwa
kumnajisi (kumlawiti) mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka minne huko
Shehia ya Piki Wilaya hiyo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi baba mzazi wa mtoto huyo alisema
mtuhumiwa alimchukuwa mwanawe hadi Bahanasa na kuingia kwenye gari ya
abiri na kumpeleka bonde la Hindi na kumfanyia ulawiti.
Alisema mtuhumiwa ni mgeni katika shehia hiyo, alikwenda kwa kutembea,
ingawa alichokifanya ni kumchukua mtoto wake na kwenda kufanyia kitendo
cha ulawiti, jambo ambalo linamtia huzuni kila anapofikiria.
“Huyo mtuhumiwa ni mgeni hapa kijijini kwetu, alipoona tu washamzoea
watoto ndipo alipoamua kumchukua mwanangu kwenda kumlawiti na huko kwao
tumesikia kaondoshwa kwa kuwafanyia watoto kitendo hicho”, alisema baba
huyo.
Kwa upande wake mama wa mtoto, alisema aliondoka na kwenda mazikoni,
ambapo mara baada ya kufika alipigiwa simu na kuambiwa kuwa mwanae
amemfuata na ndipo alipofanya haraka ya kurudi, ingawa alipofika
hakumkuta.
“Alimpelea katika bonde la Tangoni – Hindi na wakati anamlawiti
wakatokea watoto wanaochuma mabungo na mtuhumiwa akakimbia, ndipo
walipomuuliza anapoishi na kusema na wakamleta nyumbani”, alisema mama
huyo.
Alieleza mara baada ya kufika mtoto wao walimuhoji na kusema kuwa kaka
Bakar, alimchukua na kwenda kumfanyia kitendo cha ulawiti na kisha kumpa
maandazi, ambapo aliporudi alikuwa nayo kwenye mfuko.
“Walikuja wazazi wa upande wa mtuhumiwa tufanye suluhu ili tusiifikishe
kesi Polisi, lakini kwa kitendo alichofanyiwa mwanangu siwezi kusamehe,
kwani huu ni ukatili”, alisema mama huyo.
“Huyu mtoto ana kawaidi ya kucheza na mwanangu, sasa alikuja mwanangu na
kilio na kuniambia kaka ananikimbia, nikatoka nje nikamwita lakini na
mtuhumiwa ikawa anamwita, sasa ikawa kama tunavutiana, ingawa sikuwa na
wasiwasi nae nikaona labda anamfuata tu kwa vile washamzoea”, alisema
jirani wa mtoto huyo.
Nae, kijana mmoja anaeishi mtaa huo, alisema alimshuhudia mtuhumiwa
akiingia kwenye gari na mtoto huyo maeneo ya Bahanasa na kuteremka
Mzambarauni majira ya saa 3:00, ingawa hakujua alikompeleka kutokana na
yeye alikuwa anaenda Wete.
“Mimi sikufanya wasiwasi maana nilijua ni mdogo wake wa maduguni, kwa
hiyo niliporudi ndio nikapata taarifa hiyo na ndipo nilipokumbuka wakati
nilipomuona anapanda nae gari”, alisema kaka huyo.
Mratibu wa shehia ya Piki, Bikombo Shazil Makame, alisema tukio hilo
limetokea katika shehia yake na tayari wameshalifikisha kituo cha
Polisi Wete, ambapo aliwataka wazazi kuwa mstari wa mbele kwenda kutoa
ushahidi mahakamani, ili kesi iweze kupata hatia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Haji Khamis Haji, alisema
tukio hilo lilitokea Januari 2 mwaka huu saa 6:00 mchana huko Piki,
mtuhumiwa huyo alimnajisi mtoto wa kiume mwenye miaka minne shehia ya
Piki Wilaya ya Wete.
Kamanda huyo, alisema mtuhumiwa huyo ameshakamatwa na Jeshi hilo
linaendelea na upelelezi, ambapo watampeleka mahakamni mara baada ya
uchunguzi kukamilika kujibu tuhuma zinazomkabili.
Matukio ya udhalilishaji kwa watoto ikiwemo ulawiti yamekuwa
yakiongezeka kila siku, kutokana na sababu mbali mbali, ikiwemo
wanajamii kukataa kutoa ushahidi pamoja na kesi kukaa muda mrefu
mahakamani bila ya kupatiwa hukumu.
COMMENTS