Mwishoni mwa wiki iliyopita, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ameitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutenda haki katika kutangaza wash...
Mwishoni
mwa wiki iliyopita, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ameitaka Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutenda haki katika kutangaza washindi wakati wa
uchaguzi.
Majaliwa
ameyasema hayo Alhamisi iliyopita mjini Dodoma, alipokuwa akijibu swali
la Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Devotha Minja, wakati wa kipindi
cha ‘maswali kwa Waziri Mkuu.’
Minja
akatoa mfano kuwa uchaguzi mdogo uliofanyika katika kata 43 Novemba
mwaka jana, ulionekana kuwa na dosari nyingi akidai Chadema ilihujumiwa
kutokana na NEC kuwatangaza wagombea wa udiwani kadhaa kupitia CCM kuwa
washindi licha ya kuwa walishindwa kwa kura nyingi.
Tunalazimika
kuunga mkono tamko la Waziri Mkuu Majaliwa na kuisihi NEC na wadau
wengine kutekeleza wajibu wao ipasavyo hasa katika kuwatangaza washindi
wa uchaguzi, ili matokeo husika yasiwe chanzo cha mifarakano.
Suala
la uchaguzi huru linagusa maeneo na wadau wengine wakiwamo wanasiasa,
polisi, wasimamizi wa uchaguzi, japo kuwataja kwa uchache.
Kwa
hali hiyo, tamko la Waziri Mkuu Majaliwa linaweza kuvuka mipaka ya NEC
na kuwahusisha wadau wakiwamo tuliowataja hapo awali, na tume hiyo
ikabaki kuwa mratibu katika kuhakikisha mshindi anayetokana na kura
nyingi, ndiye anayetangazwa.
Mathalani,
kama wanasiasa watashindwa kutumia hoja zenye ushawishi ili waungwe
mkono na kupata kura nyingi, badala yake wakashirikiana na wadau wengine
kupanga na kutekeleza njama za kuuhujumu uchaguzi husika, haipaswi
kuvumilika.
Ama
kama polisi watakubali kutumika kwa namna yoyote, na mdau yeyote katika
uchaguzi unaofanyika nchini, kusimamia na kuuhujumu uchaguzi husika,
hawatapaswa kuvumiliwa.
Ndivyo
inavyopaswa kufanyika kwa wadau wote, kwa maana uzoefu unaonesha kuwa
uchaguzi ni miongoni mwa vyanzo vikuu vinavyosababisha na kuchochea
vurugu na mifarakano kwa jamii.
Tanzania
imewahi kushuhudia machafuko yaliyotokea Zanzibar baada ya Uchaguzi
Mkuu wa mwaka 2000, na kusababisha raia wa nchi hii kukimbilia kwenye
kambi ya wakimbizi Shimoni nchini Kenya.
Kadhalika,
kumekuwapo vurugu katika chaguzi kadhaa, hata kama zikiwa katika
kiwango kidogo, lakini zinaathiri taswira ya nchi, mahusiano na amani ya
nchi. Tanzania isiyokuwa na migogoro inayotokana na matokeo ya
uchaguzi, inawezekana.
Tunarejea
kuisihi NEC, irejee na kulitumia agizo la Waziri Mkuu Majaliwa kama
mwongozo wa kuliweka Taifa katika hali ya amani, umoja na mshikamano kwa
kuwatangaza washindi halali wa uchaguzi na si vinginevyo.
Uchaguzi
wowote wa viongozi na wawakilishi wa wananchi nchini, unawahusisha raia
wa Tanzania wenye sifa zinazotambuliwa kwa mujibu wa Katiba ya nchi.
Hivyo,
Watanzania wanaposhiriki uchaguzi ili wachaguliwe na Watanzania
kuwaongoza ama kuwawakilisha, isiwe chanzo cha mifarakano katikati yao
na namna ya kuepukana na hatari hiyo ni kwa NEC kutekeleza agizo la
Waziri Mkuu Majaliwa.
COMMENTS