Serikali imetoa muda wa wiki mbili kwa Kampuni Hodhi ya Rasimali za Reli (RAHCO) kusafisha maeneo yote yaliyobomolewa na kampuni hiyo i...
Serikali imetoa muda wa wiki mbili kwa Kampuni Hodhi ya Rasimali za Reli (RAHCO) kusafisha maeneo yote yaliyobomolewa na kampuni hiyo ikiwemo stendi kuu ya mabasi Dodoma.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Kangi Lugola ametoa agizo hilo mkoani Dodoma alipotembelea na kukagua eneo la stendi hiyo ambalo lilibomolewa na RAHCO kwa ajili ya kupisha ujenzi wa reli ya kisasa.
“Kulikuwa na zoezi la ubomoaji katika eneo hili la stendi lakini baada ya uboaji hakuna usafi wowote uliofanyika na kampuni ya RAHCO ambayo ndio iliyofanya zoezi hilo la ubomoaji,” alisema Lugola.
Aliendelea kwa kusema eneo hilo limeachwa likiwa na mabaki ya mbao, matofali, misumari, na mabati yakiwa yameenea kila eneo hivyo kulifanya eneo hilo la stendi kuwa chafu.
Hivyo basi Mhe. Lugola amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa RAHCO kuhakikisha analisafisha eneo hilo na kulizungushia uzio ili kuzui kuendelea kuchafuliwa kutokana na eneo hilo kuwa wazi.
Lugola amesema Mji wa Dodoma kupitia Manispaa yake una maeneo ambayo yametenga kwa ajili ya stendi, hivyo stendi itahamishiwa eneo hilo lililotengwa mara tu baada ya kukamilika.
Aidha mmoja wa wafanyabiashara wa eneo hilo Ndugu Zakaria Mmari aliuliza juu ya kufikiriwa kwa wafanyabiashara wa eneo hilo kuendelea kufanya biashara mpaka pale stendi mpya itakapokamilika.
“Yote mliyoyaeleza nimeyachukua na nitaenda kufanyia kazi na mtajulishwa majibu ya ombi lenu,” alijibu Lugola.
COMMENTS