Serikali mkoani Rukwa imesema inafanya mkakati wa kuwamaliza panya wote porini kwani wamekuwa ni sababu ya wakazi wa mkoa huo kuchom am...
Serikali mkoani Rukwa imesema inafanya mkakati wa kuwamaliza panya wote
porini kwani wamekuwa ni sababu ya wakazi wa mkoa huo kuchom amoto
misitu kwa nia ya kutafuta panya ili watumie kama kitoweo
Akizungumza jana wakati wa kampeni ya upandaji miti kwa lengo la
kuhifadhi mazingira katika Kijiji cha Mpwapwa, kata ya Mpwapwa, Wilayani
Sumbwanga mkuu wa mkoa huo Joachim Wangabo alimuagiza mkuu wa wilaya ya
Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule ahakikishe anatafuta dawa ya kuua panya
porini ili kuokoa miti kwani baadhi ya watu wamekuwa wakichoma moto
misitu kwa ajili ya kuwindaji wa panya.
Alisema kuwa amesikia changamoto hiyo ya uchomaji wa misitu kwa sababu
ya uwindaji wa panya kutoka kwa vijana mbalimbali wanaojishughulisha na
mashamba ya upandaji miti pamoja na taarifa iliyosomwa na mkurugenzi wa
halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga juu ya changamoto za kuendeleza
misitu.
“DCnakuagiza tafuta dawa ya panya, wauliwe huko mashambani na porini ili
panya wasiwepo na miti iokoke, mbona hamshangilii? hawa panya tutawaua
kwa sumu huko mashambani wasiwe chanzo cha moto ambao mnachoma huko
kuwatafuta wafie huko huko mashimoni msiwapate,” alisema.
Pia alimuagiza mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo kuhakikisha
anasimamia sheria ya hifadhi ya mazingira na kuwawajibisha wote
wanaohusika na uharibifu wa mazingira ambapo mkuu huyo wa mkoa alitoa
miche 850 kwa kaya 850 za kijiji cha Mpwapwa ili ipandwe kila kaya mti
mmoja.
Awali akisoma taarifa mkurugenzi wa halmashauri hiyo John Msemakweli
alibainisha kuwa miongoni mwa changamoto ni muitikio mdogo wa uhifadhi
wa mazingira pamoja na mila na tamaduni za wananchi za uwindaji wa panya
hali inayosababisha uchomaji wa misitu wakati wa kiangazi.
“Changamoto nyingine ni baadhi ya viongozi wa serikali ya kijiji
kujihusisha na uuzajia wa maeneo yaliyotengwa kwaajili ya hifadhi ya
Kijiji na usimamizi mdogo wa sheria ndogo za vijiji katika utunzaji wa
misitu,”alisema.
Katika msimu wa mwaka 2017/2018 hadi 30/1/2018 halmashauri ya wilaya ya
Sumbwanga imepanda miti 830,527 ambayo ni sawa na asilimia 55.4 na ina
misitu 92 yenye ukubwa wa hekta 49,179.6.
Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho Steven Sichula alilipokea kwa masikitiko
agizo hilo la mkuu wa mkoa kwani alisema kuwa sio haki kuwamaliza
panya wote kwani nao ni viumbe hai wanahitaji kuishi na ni kitoweo kwao
kwani wanapata protini ambapo alishauri utafutwe utaratibu mwingine wa
kukomesha tabia hiyo lakini si kuwaua panya wote.
COMMENTS