Sakata la Klabu ya Yanga kuzuiliwa kufanya mazoezi katika uwanja wa Taifa lililotokea siku ya jana (Alhamisi) limezua sura mpya na kufa...
Sakata la Klabu ya Yanga kuzuiliwa kufanya mazoezi katika uwanja wa
Taifa lililotokea siku ya jana (Alhamisi) limezua sura mpya na kufanya
Waziri mwenye dhamana Dkt. Harrison Mwakyembe kulitolea ufafanuzi
Bungeni.
Dkt. Mwakyembe ametoa ufafanuzi huo leo (Ijumaa) katika mkutano wa 10
kikao cha nane cha Bunge kilichomalizika kwa kuhairishwa shughuli zake
mpaka Aprili 03, mwaka 2018 mjini Dodoma wakati alipokuwa akijibu swali
la Mbunge wa Mchinga (CUF), Hamidu Bobali ambapo aliitaka serikali
kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo iingilie kati
suala la timu za Tanzania zikienda kucheza kimataifa huwa zinawekewa
zengwe lakini wao wakija kucheza huku wanapewa kipaumbele baadhi ya
vitu.
"Haturuhisiwi hicho kiwanja kukitumikisha kubeba michezo zaidi ya mitatu
kwa wiki moja na endapo utafanya hivyo unaingiza uswahili na hata
kikiharibika huwezi kwenda kudai kwa mtu aliyekupa 'guranty' kwamba
kitaka zaidi ya miaka 10", amesema Dkt. Mwakyembe.
Pamoja na hayo, Dkt. Mwakyembe ameendelea kwa kusema "kwa hiyo wiki hii
tuna mechi mbili muhimu kesho (Jumamosi) wanacheza Yanga dhidi ya St.
Louis na kesho kutwa wanaingia Simba SC (Jumapili) kucheza na timu
kutoka Djibout. Kanuni za kimataifa zinataka timu ngeni hiyo ya
kimataifa lazima ifanye mazoezi katika kiwanja ambacho kitachezwa mechi
hiyo lakini hata FIFA wanatambua hicho kiwanja ni cha timu za hapa
nchini. Kwa hiyo Yanga na Simba wanaufahamu vizuri uwanja huo ndio maana
wakapewa kipaumbele wageni ili waweze nao kuujua".
Aidha, Dkt. Mwakyembe amesema anahisi kuna uswahili umeshaanza kuingia
katika uwanja wa Taifa na kutaka baadhi ya watu kushughulikiwa.
"Uswahili umeshaanza kuingia katika uwanja wetu wa Taifa, na mimi
nashukuru kwa haya maneno niliyoyapata nadhani kuna vijana wangu pale
wanahitaji wadhibitiwe kwa kweli. Kwa hiyo nataka nifafanue kwamba ni
haki ya wageni wapewe nafasi ya kufanya mazoezi na sisi tukafanyie
katika viwanja vingine", amesisitiza Dkt. Mwakeymbe.
Kwa upande mwingine, Dkt. Mwakyembe amesema ili uwanja huo uweze
kutunzika katika mazingira mazuri bila ya kuharibiwa jambo lolote ndani
ya miaka 10 ni lazima yawepo masharti ya utumiaji.
COMMENTS