Katibu Mkuu wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe akipata maelezo namna wadudu wanavyoshambulia zao la pamba kutoka kwa mkaguzi w...
Katibu Mkuu wizara ya Kilimo Mhandisi
Mathew Mtigumwe akipata maelezo namna wadudu wanavyoshambulia zao la
pamba kutoka kwa mkaguzi wa pamba wilaya ya Bariadi Alfred Chagula,
walipotembelea mashamba ya wakulima jana Mbiti.
Katibu Mkuu wizara ya Kilimo Mathew
Mtigumwe (mwenye miwani) akimsikiliza mkulima wa pamba Tindigwe Masuke
wa kijiji cha Mbiti alipokuwa akiongelea juu ya uhaba wa dawa,
unaowakabili wakulima hao.
Serikali imewahakikishia wakulima wa
pamba Mkoani Simiyu kuwapatia pembejeo za kilimo ili kukabiliana na
wadudu waharibifu ambao wameanza kushambulia zao hilo.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wizara
ya Kilimo, Mhandisi Mathew Mtigumwe alipofanya ziara ya kukagua
mashamba ya wakulima na kujionea changamoto zinazowakabili, ikiwemo
mazao yao kushambuliwa na wadudu katika maeneo mbalimbali mkoani hapa.
"Tumeanza kusambaza pembejeo kwa
wakulima mkoani Simiyu baada ya kuona mahitaji ya dawa ni makubwa…awali
tulipanga kusambaza chupa milioni 1.8, Lakini mahitaji yamekuwa ni
makubwa tumeongeza na kufikia chupa milioni 2 ili kusuru zao
hilo",alisisitiza Katibu mkuu.
Aliongeza kuwa wizara ya kilimo
imesambaza watalamu 30 nchini ili kusaidiana na wataalamu kilimo ngazi
ya mkoa, wilaya na kata katika kutoa elimu kwa wakulima juu ya matumizi
sahihi ya dawa, pia namna ya kukabiliana na wadudu waharibifu wa mazao.
Mtigumwe aliwataka wataalamu wa kilimo
kutoa elimu kwa wakulima juu ya matumizi sahihi ya pembejeo za kilimo
ili kuhakikisha dawa zinazosambazwa zinatumika ipasavyo.
Tindigwe Masuke mkulima wa Pamba kijiji
cha Mbiti alisema kuwa dawa zinazosambazwa na serikali hazitoshelezi
mahitaji ya wakulima ambao wahamasika kulima, wamekuwa wakipata
kidogokidogo hali inayowafanya kushindwa kuwakabili wadudu wa pamba.
Kwa upande wake Meneja wa Bodi ya pamba
kanda ya Ziwa, Jones Bwahama alisema kuwa serikali kwa kusirikiana na
bodi ya Pamba imeleta timu ya wataalamu saba katika mkoa wa simiyu ili
kusaidia na maafisa ugani kuelimisha wakulima jinsi ya matumizi sahihi
ya pembejeo.
Mkoa wa Simiyu unahitaji chupa za dawa
1,810,839 huku kukiwa na jumla ya wakulima wa pamba 309,511 ambao
wamelima ekari 602,409 likitarajiwa kuzalisha tani 421,686.3 za pamba
kwa wastani wa kilo 700 kwa ekari moja.
COMMENTS