NA CLEMENT MAGEMBE DAR ES SALAAM Sakata la kuwaondoa kazini watumishi waliokuwa na vyeti `feki’ linadaiwa kuitesa Taasisi ya Sarat...
NA CLEMENT MAGEMBE
DAR ES SALAAM
Sakata
la kuwaondoa kazini watumishi waliokuwa na vyeti `feki’ linadaiwa
kuitesa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) jijini Dar es Salaam,
kwa wafanyakazi waliobaki kuzidiwa na utoaji huduma kwa wahitaji
hususani wagonjwa.
Taarifa
zimedai kuwa kitengo kilicholemewa zaidi ni watumishi wa chumba cha
maiti (mochwari) ambao wako wawili, baada ya wenzao watatu kuondolewa
kazini kutokana na kuwa na vyeti `feki’ vya kidato cha nne.
Vyanzo
vyetu kutoka ORCI vimeeleza kuwa kutokana na upungufu huo, inawalazimu
wafanyakazi wa taasisi hiyo kufanya kazi kwa muda mrefu bila kupumzika
na hivyo kujikuta katika mazingira yanayohatarisha afya zao.
Kwa
mujibu wa vyanzo hivyo, kitengo kingine kilichoelemewa katika utoaji wa
huduma ni tiba ya mionzi ambapo idadi ya wahudumu haikidhi wingi wa
wagonjwa wanaofika kutibiwa.
“Tumelazimika
kuwapa wagonjwa ratiba ya siku za kuanza matibabu, kwa kuwa wagonjwa ni
wengi mno kuliko wahudumu wa afya,” amesema mmoja wa wafanyakazi wa
taasisi hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Hata
hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dk. Julius Mwaiselage, amekana
kuhusu taasisi hiyo kuzidiwa katika utoaji wa huduma baada ya waliokuwa
wafanyakazi wake kuondolewa katika kashfa ya vyeti ‘feki’.
“Ni
kweli kuna upungufu wa watumishi lakini siyo kwa kiwango cha
kusababisha kuelemewa ama kushindwa kutoa huduma,” amesema Dk.
Mwaiselage.
Dk. Mwaiselage ORCI hivi sasa ina watumishi 246 kati ya 300 wanaohitajika hivyo kusababisha mahitaji ya watumishi 54.
Kwa
mujibu wa Dk. Mwaiselage, watumishi walioondolewa katika taasisi hiyo
kutokana na kashfa ya vyeti feki ni 15 na kwamba watumishi 13
wameshaajiriwa kuziba nafasi hizo.
Pia
Dk. Mwaiselage amesema ORCI imepata bajeti ya kuajiri watumishi 42
katika mwaka huu wa fedha, hivyo wanatarajia kuondokana na upungufu huo.
COMMENTS