Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema amehoji sababu za Bunge kutogharamia matibabu ya Tundu Lissu aliyepo nchini Ubelgiji ...
Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema),
Godbless Lema amehoji sababu za Bunge kutogharamia matibabu ya Tundu
Lissu aliyepo nchini Ubelgiji tangu Januari 7, 2018 akipatiwa tiba ya
mazoezi.
Lema ametoa kauli hiyo leo Februari 8, 2018 bungeni mjini Dodoma wakati
akichangia taarifa za utekelezaji wa shughuli za kamati za Bunge za
Utawala na Serikali za Mitaa, Katiba na Sheria na Sheria Ndogo.
Lissu ambaye ni mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) alishambuliwa kwa
zaidi ya risasi 30 akiwa ndani ya gari lililokuwa nje ya makazi yake
mjini Dodoma Septemba 7 mwaka jana, kupatiwa matibabu Hospitali ya Mkoa
wa Dodoma ambapo siku hiyo hiyo alihamishiwa Hospitali ya Nairobi,
Kenya.
Alipelekwa Ubelgiji Januari 7 kwa ajili ya tiba ya mazoezi na mara
kadhaa familia yake imelishutumu Bunge kuwa kimya kuhusu matibabu ya
mbunge huyo ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
Katika mchango wake, Lema alianza kwa kutoa pole kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai aliyedai kuwa yupo nchini India kwa matibabu.
“Mheshimiwa Spika anatumia fedha za Serikali kupata matibabu na mbunge
Lissu tumeendelea kumtafutia fedha za matibabu mitaani tena kwa
mkopo,”amesema Lema.
Amebainisha kuwa kitendo cha Ndugai kutibiwa na fedha za Serikali huku
Lissu ambaye ni mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni akishindwa
kupewa msaada na Bunge ni jambo ambalo halikubaliki.
Wakati akieleza hayo, alikatishwa na Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge
akimtaka ajielekeze kwenye hoja tatu za taarifa za kamati huku mbunge wa
Kishapu (CCM), Suleiman Nchambi akisema bima walizonazo wabunge
zinawawezesha kupata matibabu.
“Kama hawana mawasiliano mazuri na Bunge nawashauri na nawapa taarifa wawasiliane na ofisi ya Bunge,” amesema Nchambi.
Kauli ya Nchambi iliibua mvutano bungeni, huku mbunge wa Tarime Vijijini
(Chadema), John Heche akisikika akisema kauli ya mbunge huyo wa Kishapu
ni sawa na kucheza na uhai wa mtu.
Kufuatia hali hiyo, Chenge aliingilia kati na kuwatuliza wabunge hao kwa
kuwataja kwa majina, akiwemo Heche na mbunge wa Iringa Mjini (Chadema),
Mchungaji Peter Msigwa.
Mwenyekiti huyo alipomtaka Lema kuendelea na mchango wake, mbunge huyo
aliendelea kuzungumzia matibabu ya Lissu na kubainisha kuwa suala hilo
linahusu utawala bora, si vinginevyo kama inavyodaiwa na Nchambi.
“…, Huyu (Nchambi) anasimama anaongea mzaha kuna watu wamepotea mmoja
anaitwa Ben Saanane (msaidizi wa mwenyekiti wa Chadema-Freeman Mbowe)
haya ni mambo yanayohusu utawala bora na sheria,” amesema Lema.
Amesema kujadili matibabu ya Lissu na masuala ya utekaji hawana lengo la kushutumu, bali ni kutaka mambo yarejee katika mstari.
Licha ya Lema kuendelea kuchangia taarifa hizo za kamati huku
akikatishwa mara kwa mara, muda wake ulipomalizika alitakiwa na Chenge
kuketi ili kumpisha mchangiaji mwingine.
Na Sharon Sauwa, Mwananchi
COMMENTS